CHUO CHA KIMATAIFA CHA UVUVI KUJENGWA BAGAMOYO
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatarajia kujenga chuo kipya cha Uvuvi chenye hadhi ya kimataifa kitakachokuwa chini ya Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi nchini (FETA) kampasi ya Mbegani Bagamoyo mkoani Pwani.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt.Bashiru Ally kakurwa alipotembelea kampasi hiyo Februari 12, 2026 ambapo ameeleza kuwa chuo hicho kitakuwa cha kisasa zaidi kwenye eneo la utoaji wa mafunzo ya uvuvi, miundombinu ya kufundishia, mifumo ya kiteknolojia, vifaa vya kufundishia na uwezo wa wakufunzi.
"Nafurahi kusikia mmeunda kamati ya mazungumzo baina ya Chuo kwa niaba ya Wizara na Mamlaka ya bandari na kamati hiyo isiwe na picha ya chuo kilichojengwa wakati Mwalimu Nyerere anahangaika kujenga Taifa bali kiwe na hadhi inayofanana na kumbukizi ya baba wa Taifa" Amesema Balozi Dkt Bashiru.
Mbali na ujenzi wa chuo hicho, Balozi Dkt. Bashiru amesema Serikali inatarajia kununua meli mpya ya uvuvi kwaajili ya shughuli za mafunzo.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Prof. Mohammed Sheikh amesema kuwa shughuli za uvuvi nchini haziwezi kufanyika bila kuwa na mafunzo yatakayowawezesha wataalam hususan wale wa ndani kufanya shughuli hizo kwa ufanisi na uaminifu.
“Wataalam wa ndani ni silaha, usalama na ujasiri na wakiwa wazalendo hawawezi kudanganywa na sio rahisi kutumika kuhujumu maslahi ya nchi hivyo chuo hiki ni hazina kwa Taifa na sekta na kila unapopita ukikuta wavuvi basi asilimia 75 wametoka FETA” Ameongeza Mhe.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa FETA Dkt.Semvua Mzighani amesema kuwa katika kutekeleza majukumu yake Taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na Baraza la Elimu nchini,vyuo vikuu, vyuo vya kati, shule za msingi na Sekondari na Wakala nyingine kama vile TASAC, jeshi la wanamaji na Mamlaka ya misitu nchini.
“Pia tunashirikiana na mashirika ya kikanda na kimataifa na vile vile tuna miradi ambayo tunaitekeleza kwa kutumia mgao wa kila mwezi tunaopatiwa na Serikali na kwa kutumia fedha za wahisani kwa mfano sasa hivi tuna mradi wa TASFAM ambao utatupatia fedha za kununulia meli moja ya mafunzo” Amesema Dkt. Mzighani.