FETA YAENDESHA MAFUNZO YA SIKU SABA KWA WANUFAIKA WA BOTI ZA UVUVI.
Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Kampasi ya Mbegani, Bagamoyo kupitia mradi wa TASFAM imeendesha mafunzo ya siku saba kuanzia tarehe 14 hadi 20 Mwezi Mei, 2026 kwa wanufaika 14 wa boti za uvuvi zilizotolewa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia mkopo wenye masharti nafuu .
Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uelewa washiriki kuhusu suala zima la usalama kwenye maji, utunzaji wa boti na usimamizi wa sheria na kanuni za uvuvi.
Akiongea wakati wa kuwatunuku vyeti washiriki hao, Naibu Mkuu wa FETA Bi Merisia S. Mparazo amewaasa washiriki kutumia ujuzi katika utendaji wao wa kazi za kila siku ili waweze kunufaika na mkopo huo.
Aidha, amewaasa washiriki kuwa mabalozi wa kusambaza ujuzi walioupata kwa wananchi wengine ambao hahajapata fursa ya kushiriki kwenye mafunzo.
Pia, ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa mafunzo kama hayo kwa wavuvi kadri uwezesho utakavyopatikana ili jamii za pwani ziweze kufufaika na uwepo wa Sekta ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu kwa ujumla.
Naye Mratibu wa mafunzo ya muda mfupi ambae pia ni mratibu wa Mradi wa TASFAM upande wa FETA Bw Arnold Mbunda amefafanua kuwa kwa awamu ya kwanza, washiriki 14 kutoka katika mikoa ya ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi wamejengewa uwezo na kwamba kupitia mradi huu bado kuna fursa za kuendesha mafunzo kama hayo kwa wadau wengine wa sekta ya uvuvu katika ukanda huo.
Aidha amefafanuwa kuwa mafunzo yaliyotolewa ni pamoja na: Huduma ya kwanza; Jinsi ya kuishi ukisubiri msaada ndani ya maji; Jinsi ya kupambana na moto pamoja; na Jinsi ya kuokoa mtu au kujiokoa mwenyewe ukiwa kwenye maji.
Nao washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru Serikali, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na FETA kwa kutoa mafunzo hayo yenye tija kwa jamii za wavuvi na wameahidi kutumia ujuzi walioupata kufanya kazi zao kwa weledi huku wakitunza boti walizokopeshwa na kusimamia rasilimali za uvuvi na mazingira ya bahari kwa ujumla.