Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA)

PROFESOR SHEIKH AWATAKA WAKAGUZI WA MAZAO YA UVUVI  KULISAIDIA TAIFA KUSAFIRISHA KWA WINGI MAZAO YA UVUVI NJE YA NCHI.

Imewekwa: 09 April, 2026
PROFESOR SHEIKH AWATAKA WAKAGUZI WA MAZAO YA UVUVI  KULISAIDIA TAIFA KUSAFIRISHA KWA WINGI MAZAO YA UVUVI NJE YA NCHI.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh amewataka wakaguzi wa mazao ya uvuvi kufanya kazi zao kwa ubora ili kulisaidia Taifa kuongeza kiwango cha  mazao ya uvuvi yanayosafirishwa nje ya nchi.

Prof Sheikh ametoa kauli hiyo 8 April, 2026 wakati akizindua mafunzo ya siku tano kwa maafisa wakaguzi wa mazao ya uvuvi 25 yaliyoandaliwa na  Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kwa kushirikiana na Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO).

"Takwimu zinaonesha kwasasa tunasafirisha tani 60,000  pekee za samaki kwenda nje ya nchi hivyo uwepo wa mafunzo haya uwe chachu ya kuongeza ubora utakaosaidia Taifa kuongeza kiasi cha samaki kinachopelekwa nje ya nchi" Amesema Prof. Sheikh

Akiongea Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Dkt Semvua Mzighani amesema Mafunzo haya yamelenga kuwajengea uwezo  maafisa ukaguzi wa mazao ya uvuvi juu ya taratibu za ukaguzi wa mazao ya uvuvi pamoja na  viwango vya ubora vya kitaifa,kikanda na kimataifa.

Pia amewasihi washiriki wa mafunzo kuzingatia mafunzo watakayopatiwa na elimu watakayoipata kupitia mafunzo hayo ikawasaidie wananchi katika maeneo yao.

Awali Mratibu wa mafunzo hayo Mkufunzi Anold Mbunda amesema hii ni awamu ya kwanza ya mafunzo ambapo imejumuisha washiriki toka ukanda wa pwani, awamu ya pili ya mafunzo haya itafanyika mkoani Kigoma ambapo itahusisha washiriki kutoka kanda ya ziwa.