SERIKALI YAKABIDHI BILIONI 7 KWA VIJANA 308 MRADI WA BBT UVUVI.
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekabidhi hundi ya shilingi Bil. 7 kuwezesha mitaji kwa vijana waliohitimu mafunzo ya program ya Jenga Kesho iliyo Bora kwa upande wa sekta ya Uvuvi (BBT-UVUVI) ambapo zitatumika kwenye shughuli za ukuzaji viumbe maji.
Akizungumza kabla ya kukabidhi hundi hiyo Mgeni rasmi wa hafla hiyo ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe. Joel Nanauka amesema kuwa fedha hizo zinatolewa kama mikopo yenye mashart nafuu kwa vijana kwa ajili ya kuwezesha mitaji, vifaa, pembejeo muhimu za ukuzaji viumbe maji pamoja na posho ya kujikimu kwa washiriki.
"Program hii haitaishia tuu hapa , itaenda ukanda wa pwani na mtwara kwani mradi wenyewe una sura ya ukuzaji wa uchumi wa buluu ” Amesema Mhe. Nanauka
Aidha amewakumbusha vijana wanufaika kuwa hii ni mikopo, wana wajibu wa kufanya marejesho kwa uaminifu ili fedha zinazopatikana ziweze kuwasaidia vijana wengine ambao wana uhitaji.
Naye Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Ng'wasi Kamani amesema kuwa uwezeshaji wa vijana hao ni sehemu ya mikakati ya wizara ya kuongeza uzalishaji pamoja na kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la Taifa sambamba na utoaji wa ajira nchini.
"Takwimu zinaonesha kuwa kwa sasa kila mtu anakula samaki kilo 7.9 kiasi ambacho kiko chini ukilinganisha na hitaji la shirika la chakula na Kilimo Duniani (FAO) kinachotaka kila mtu kula kilo 20 za samaki kwa mwaka hivyo hali hiyo inaonesha fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji kupitia miradi ya ufugaji samaki kwenye vizimba ili kukidhi hitaji la ulaji wa samaki nchini" Ameongeza Mhe. Kamani.
Akizungumza kwa niaba ya katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Agness Meena, Naibu katibu Mkuu anayeshughulikia Uvuvi Prof. Mohammed Sheikh amesema kuwa program ya jenga kesho iliyobora (BBT Uvuvi) ni mpango unaolenga kuongeza ushiriki wa vijana katika shughuli za uvuvi na ukuzaji viumbe maji ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi sambamba na kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana.
"Fedha hizi zinatarajiwa kuwawezesha mitaji vijana 308 ambapo vijana 160 watatekeleza miradi ya ufugaji samaki kwenye vizimba, vijana148 watatekeleza miradi ya ufugaji jongoo bahari, kilimo cha mwani pamoja na unenepeshaji wa kaa” Amesema Prof. Sheikh.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Dkt Semvua Mzighani ambao ndio watekelezaji wakuu wa mradi huo amesema kuwa Taasisi yake imejiandaa kitaalam kusimamia, kuratibu na kuhakikisha mradi huo unafanikiwa katika viwango vilivyokusudiwa.
"FETA ndio itasambaza pembejeo muhimu ikiwa ni pamoja na vifaranga vya samaki na chakula cha samaki lakini pia itasimamia uwekaji wa miundombinu kama vizimba pamoja na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya mradi" Amesema Dkt Mzighani.
Fedha zilizokabidhiwa leo ni sehemu ya shilingi Bilioni 200 zilizoahidiwa kutolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe. Samia Suluhu Hassan ambapo utekelezwaji wake utaongeza ajira zaidi za watanzania 4600 walioajiriwa kwenye viwanda 64 vya kuchakata mazao ya uvuvi nchini huku pia ikitarajiwa kuongeza uzalishaji wa samaki uliofikia takribani tani 599,199 kwa sasa.