Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA)

VIJANA 85 MKOANI GEITA WAKABIDHIWA  MITAJI YA UFUGAJI SAMAKI KWA NJIA YA VIZIMBA.

Imewekwa: 27 November, 2026
VIJANA 85 MKOANI GEITA WAKABIDHIWA  MITAJI YA UFUGAJI SAMAKI KWA NJIA YA VIZIMBA.

Vijana hao ni wale waliohitimu mafunzo ya Jenga kesho iliyo Bora maarufu kama BBT Uvuvi.

Akiongea wakati wa hafla ya kuwakabidhi mitaji hiyo iliyofanyika Mkoani Geita Wilayani chato 20,Novemba 2026 Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe. Alexander Mnyeti amewataka vijana hao kusimamia mradi wao kwa weledi mkubwa ili waweze kupata tija iliyokusudiwa.

"Acheni kujiona mabosi, simamieni wenyewe huu mradi kwa weledi mkubwa ili muweze kupata mavuno mazuri"

Aidha ameutaka Uongozi wa Wilaya ya Chato ambapo mradi huo unatekelezwa kuwasimamia vijana hao na kutatua changamoto ndogondogo zitakazojitokeza ili vijana hao waweze kutekeleza mradi wao vizuri na  kupata tija iliyokusudiwa. 

Nae Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa wizara ya mifugo na uvuvi ambae pia ni Mkurugenzi wa Mafunzo,Tafiti na Huduma za Ugani kutoka Wizara ya mifugo na uvuvi  Bw Samwel Mdachi ameeleza kuwa zoezi lililofanyika leo ni mwendelezo wa zoezi la ugawaji wa mitaji lililozinduliwa rasmi kitaifa Tarehe 7 Machi,2026 na Mhe Dkt. Joel Nanauka, Waziri Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana katika eneo la FETA Nyegezi .

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) ambaye pia ni Naibu Mkuu wa Wakala Taaluma, Utafiti na Ushauri Bi Merisia  Mparazo ameeleza kuwa, Wakala  imepewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa miradi ya vijana ikiwemo Kusimamia upatikanaji wa vifaa na huduma muhimu vitakavyowezesha utekelezaji wa miradi ikiwemo  vizimba vya kufugia samaki,

Kusimamia upatikanaji na upandikizaji wa vifaranga bora vya samaki, Kusimamia upatikanaji na usambazaji wa chakula bora cha samaki

Mengine ni Kusimamia ulishaji, uvunaji na uuzaji wa samaki kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu,

Kufanya tathmini na ufuatiliji wa utekelezaji wa miradi ya wanufaika na kutoa ushauri pamoja na

Kusimamia nidhamu uwajibikaji, ushirikiano na mshikamano miongoni mwa wanufaika.

Aidha, amesisitiza kuwa wakala itaendelea kushirikiana na Mkoa wa Geita na wadau wengine kusimamia vijana kutekeleza miradi yao kikamilifu ili iweze kuwa endelevu kwa lengo la kukuza kipato cha vijana, kuongeza uzalishaji wa samaki ili kuimarisha usalama wa chakula na lishe na kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Mpaka sasa jumla ya wanufaika 252 wameshapatiwa mitaji kwa kanda ya ziwa Ambapo kituo cha FETA Nyegezi Mwanza wanufaika 80, Kemondo  Bukoba wanufaika 47, Musoma Mara wanufaika 40 na Chato mkoani Geita wanufaika 85.