WAZIRI WA NCHI OFISI YA RAIS MAENDELEO YA VIJANA AONGOZA ZOEZI LA UVUNAJI NA UUZWAJI SAMAKI WA VIZIMBA FETA NYEGEZI.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe Dkt Joel Nanauka ameongoza zoezi la uvunaji na uuzaji wa samaki wa vizimba waliozalishwa na vijana wa BBT- Uvuvi kituo cha FETA Kampasi ya Nyegezi,mkoani Mwanza tarehe18 Novemba 2026.
Akiongea mara baada ya kuzindua zoezi la uvunaji wa samaki, Mhe Nanauka amesema utekelezaji wa miradi ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba kupitia Mradi wa BBT-Uvuvi ni uwekezaji mkubwa wa Serikali kwa vijana kuwawezesha kufanya shughuli za uzalishaji mali kupitia mikopo yenye mashart nafuu ili kujikwamua kiuchumi na kukuza uchumi wa Taifa.
Aidha, amewapongeza vijana wanufaika wa Program ya BBT- Uvuvi kwa kusimamia kikamilifu vizimba vyao toka tarehe 7 Machi, 2026 hadi Novemba, 2026 ambapo wameweza kuvuna samaki. Pia, amewashauri wafikirie kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kuchakata mazao ya samaki ili kuongeza thamani ya samaki wanaowazalisha.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo, Utafiti na huduma za Ugani Bw Samwel Mdachi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara ya Mifugo na Uvuvi amesema wizara yake itaendelea kuwezesha vijana wengine ambao wana utayari wa kufanya shughuli za uvuvi kadri uwezesho utakavyopatikana lengo waweze kujikwamua kiuchumi na kuchangia kwenye pato la Taifa.
Naye Naibu Mkuu wa Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA ) Bi Merisia Mparazo kwa niaba ya Mtendaji Mkuu, FETA ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuiamini FETA kusimamia vijana hawa kupitia Programu ya BBT-Uvuvi kwa kuwapatia mafunzo na utaalamu unaohitajika katika shughuli nzima ya ufugaji wa samaki.
Aidha, amebainisha kuwa licha ya kuongeza kipato cha wanufaika, samaki hawa wanaenda kuimarisha upatikanaji wa chakula na lishe kwa watanzania kwani samaki hawa wanaovunwa watasafirishwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Naye Meneja wa Kampasi ya FETA Nyegezi na Mratibu wa Programu ya BBT- Uvuvi kwa Kanda ya Ziwa Bw Jimmy Masumbuko amesema kuwa samaki waliovunwa leo ni takribani Tani 9 kutoka katika vizimba 3 ambao wanatarajiwa kutengeneza faida ya shilingi Mil 76.
Aidha, ameeleza kuwa uvunaji huu ni wa awamu ya kwanza namavuno yamepishanishwa kwa lengo la kulinda soko.
Ameongeza kuwa, mavuno yatakapokamilika kwa kituo cha Mwanza pekee wanufaika wanatarajia kuvuna takriban tani za samaki 240.